Historia Wakala wa Majengo...
Wakala wa Majengo Zanzibar ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya kifungu nambari 53 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kifungu nambari 55 cha Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya mwaka 2011, kupitia tangazo la kisheria (Legal Notice) nambari 50 la tarehe 12 Mei, 2017.
Wakala wa Majengo Zanzibar ilianzishwa kwa malengo ya kuimarisha usimamizi wa majengo ya Serikali na kuwapatia makazi yaliyo bora na nafuu viongozi na watumishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Vile vile, Wakala inawajibu wa kuratibu na kusimamia shughuli zote za ujenzi wa majengo ya Serikali kwa Unguja na Pemba na kufanya matengenezo ya majengo hayo ya Serikali na kuhakikisha ubora na viwango vya ujenzi vinafikiwa.
Kabla ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 kazi za ujenzi wa majengo ya Serikali yalikuwa yakifanywa na Taasisi ya “Public Works Department” (PWD) ambapo majengo mbali mbali ya Serikali yalijegwa kama vile Nyumba za Viongozi Mazizini, Chake Chake, Uzunguni Wete na kadhalika. Baada ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, aliekuwa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar marehemu Mzee Abeid A. Karume alianzisha sera ya kuwapatia makaazi bora wananchi wa Zanzibar ambapo mradi wa ujenzi wa nyumba za maendeleo Mijini na Vijijini kwa Unguja na Pemba ulianzishwa. Nyumba zilizojengwa kupitia mradi huo zilikabidhiwa kwa Wizara husika chini ya Idara ya Ujenzi na walipatiwa wananchi kwa ajili ya kuishi na wengine walimilikishwa ikiwa ni fidia ya nyumba zilizovunjwa kupisha ujenzi huo.
Aidha, Idara hiyo ilikuwa na jukumu la kusimamia ujenzi wa Majengo ya Serikali, kuendeleza na kukarabati majengo hayo na kuhakiki ramani za ujenzi binafsi. Vile vile Idara hii ilipewa jukumu la kusimamia majengo ya serikali na kujenga nyumba za maendeleo zilizokuwa zinajegwa sehemu mbali mbali katika Visiwa vyetu vya Unguja na Pemba kwa kukamilisha ahadi ya Mh. Rais wa Awamu ya kwanza ya kuwapatia Wananchi makazi bora na salama katika maeneo tofauti kama vile Kikwajuni, Kilimani, Michenzani, Bambi, Makunduchi, Gamba, Chake Chake, Mkoani, Wete na Micheweni. Aidha, Idara ya Ujenzi ilihusika na ujenzi wa nyumba za vijiji zilizojengwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kwenye miaka ya 1970 na 1980.
Idara iliendelea vizuri na majukumu yake hadi ilipofikia mwanzoni mwa miaka ya tisini ambapo mabadiliko ya Sera za Kiuchumi (Trade Liberalization) yalisababisha kuongezeka kwa kasi kubwa kwa ujenzi wa nyumba za aina tofauti zilizokuwa zinafadhiliwa na wafadhili wa nje (Donnar Fund Project) ambao huja na masharti mbali mbali kama kutoruhusu taasisi za Serikali kupatiwa kazi ya Ujenzi kwa miradi inayofadhiliwa na wao. Aidha, uanzishwaji wa Sera ya Nyumba ya mwaka 1985 ilipelekea kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba ambalo lilipewa majukumu ya kuwapatia na kuwawezesha Wazanzibari kumiliki nyumba na majengo mengine kwa matumizi ya makaazi, biashara, viwanda, kujenga nyumba au majengo mengine kwa ajili ya kukodisha au kuuza kwa wananchi kwa vigezo ambavyo Shirika litakavyojiwekea, kuyatunza majengo yaliopo ambayo mwanzo yalikuwa chini ya usimamizi wa Idara ya Ujenzi.
Kutokana na sababu hizo kulipelekea Idara ya Ujenzi kukosa uwezo wa kifedha, kiutaalamu na kiufundi hali iliyopelekea udhibiti usioridhisha wa ujenzi wa majengo ya Serikali hasa katika maeneo ya Mijini Unguja na Pemba. Aidha, kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya maendeleo Michenzani kuliifanya Idara ya Ujenzi kukosa shughuli maalum ya kufanya na hatimae, mwaka 2017 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliifanya idara ya Ujenzi kuwa Wakala wa Majengo kwa mujibu wa sharia ya utumishi wa umma no.2 ya mwaka 2011, kifungu nambari 55 (4), kifungu cha 53 cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kupitia tangazo la Kisheria (Legal Notice) No. 50 la tarehe 12 Mei, 2017 kwa malengo ya kuimarisha usimamizi wa majengo ya Serikali na kuwapatia makazi yaliyobora na nafuu Viongozi na Watumishi wa Serikali. Vile vile, Wakala inawajibu wa kuratibu na kusimamia shughuli zote za Ujenzi kwa majengo ya Serikali kwa Unguja na Pemba na kufanya matengenezo ya Majengo hayo ya Serikali na kuhakikisha ubora na viwango vya Ujenzi vinafikiwa.